Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar

Mhe. Hemed Suleiman Abdulla

WASIFU WA MAKAMO WA PILI

MHE. HEMED SULEIMAN ABDULLA
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

MAISHA YAKE: Mhe. Hemed Suleiman Abdulla alizaliwa 05 Aprili, 1973 katika Kijiji cha Mauwani Shehia ya Kendwa Wilaya ya Mkoani – Mkoa wa Kusini Pemba. Alibahatika kumuoa mama Sharifa Omar Khalfan na kupata Watoto watatu (3) wakiwemo; mtoto wa kiume mmoja na wakike wawili.

ELIMU NA MAFUNZO: Katika mwaka 1981-1989 alipata elimu yake ya msingi katika skuli ya Kiwani Msingi; mwaka 1990-1994 alipata elimu yake ya Sekondari katika skuli ya Fidel Castro; mwaka  1995-1996 alipata elimu ya cheti cha awali cha  Usimamizi wa Nyenzo katika Chuo Cha Uchumi na Elimu ya Biashara Tanzania; mwaka 1996-1997 alipata elimu ya cheti cha Usimamizi wa Nyenzo katika chuo hicho hicho cha Uchumi na Elimu ya Biashara Tanzania ; mwaka 2001-2004 alipata elimu ya Stashahada ya uzamili ya Uongozi wa Fedha katika chuo cha  Uongozi wa Fedha Zanzibar (ZIFA); mwaka 2005-2006 alipata elimu ya Stashahada ya uzamivu ya Uongozi wa Fedha katika Chuo Cha Uongozi wa Fedha Tanzania (IFM); mwaka 2007-2008 alipata elimu ya Shahada ya uzamili katika Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Amerika kilichopo London Uingereza; mwaka 2013-2015 alipata elimu ya Shahada ya Uzamili ya Uchumi na Fedha katika Chuo Kikuu cha Bradford kwa kushirikiana na Chuo Kikuu Mzumbe Tanzania; 2019 hadi sasa ni mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu katika Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.

UZOEFU NDANI YA SERIKALI: Katika mwaka 1992-1996 alikuwa akifanya kazi kama karani wa fedha chini ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Vijana; mwaka 1997-2004 alikuwa mshika fedha katika Wizara ya Elimu; mwaka 2004-2006 alifanyakazi kama Mkuu wa Hazina katika Wizara ya Fedha na Masuala ya Kiuchumi; mwaka 2007-2010 alifanya kazi kama Mhasibu Mkuu katika Wizara ya Fedha na Masuala ya Kiuchumi; mwaka 2011-2014 alikuwa Afisa Mdhamini katika Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko; mwaka 2014-2017 alikua Mkuu wa Wilaya ya Mkoani Pemba; mwaka 2017-2020 alikua Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba; kuanzia Novemba 2020 hadi sasa ameteuliwa kuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

UZOEFU NDANI YA CHAMA CHA MAPINDUZI: Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla kwa mujibu wa zamana za kiutendaji serikalini alishika nafasi mbalimbali ndani ya Chama Cha Mapinduzi zikiwemo nafasi ya Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Mkoani na Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Kusini Pemba.